Ndani ya Qur`ani Tukufu mara kadhaa vitendo vya kizazi kimoja pia vimehusishwa na vizazi vilivyofuata. Mathalani vitendo vya zamani vya Wana wa Israeli vimehusishwa kwa Wayahudi wa zama za Mtukufu Mtume [SAWW]. Qur`ani Tukufu inasema kwamba watu hawa wanastahili fedheha na utwezo kwa sababu walikuwa na kawaida ya kuwaua Manabii. Hilo lilisemwa kwa sababu kufuatana na mtazamo wa Qur`ani Tukufu Wana wa Israeli wa zama za Mtukufu Mtume walikuwa muendelezo na nyongeza ya wahenga wao ambao walikuwa na kawaida ya kuwaua Manabii. Si hilo tu, lakini kufuatana na mtazamo wa fikira ya pamoja walikuwa ni watu wale wale kabisa wa hapo kale ambao waliendelea kuwepo. Mwanafalsafa Mfaransa, Auguste Comte anasema: “Jamii ya binadamu inayo watu wengi zaidi waliokufa kuzidi walio hai.” Kwa maneno mengine, katika vipindi vyote vya historia watu wa kale huathiri jamii ya binadamu zaidi kuliko watu walio hai. Usemi kwamba “Wafu wanaendelea kuwatawala walio hai zaidi na wakati wote,” maana yake ni ile ile. (Kutika: Main Currents in Sociological Thought, Vol, I, p. 91)